Rais Donald Trump ameapa kumteua mtu atakaye chukua nafasi yake wiki hii, huku mgombea kiti cha urais wa chama cha Demokratic Joe Biden akipinga jambo hilo na kusema utaratibu ufanyike baada ya uchaguzi mkuu.
Katika bunge pia kuna mvutano kama huo, lakini kilicho wazi sasa ni kwamba vyama vyote viwili vinachukulia suala hilo kuwa muhimu katika kampeni ikiwa imebaki wiki sita kabla ya uchaguzi.
Kuanzia Mwishoni mwa wiki maelfu ya Wamarekani wamekuwa wakikusanyika nje ya jengo la mahakama kuu wakiweka maua na kuandika maoni yao kufuatia kifo cha Ruth Bader Ginsburg aliyefariki Ijumaa baada ya kutumikia mahakama ya juu ya taifa kwa miaka 27.
Wachambuzi wanasema kifo chake hivi sasa kinabadili muelekeo wa kampeni za uchaguzi mkuu, na kuweka nyuma masuala ya uchumi, janga la corona na ajira.
Rais Donald Trump akiwa katika kampeni yake mwishoni mwa wiki amesema atamteua mwanamke kuchukua nafasi hiyo. Wademokrats wanasema ni lazima kusubiri hadi baada ya kuapishwa kwa rais mpya mwezi Januari 2021 ili kumteua jaji mpya kama walivyofanya mnamo mwaka wa mwisho wa utawala wa Barack Obama pale Warepublican walipokata kuidhinisha uteuzi wake.
Spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi aliyeweka shada lake la maua nje ya mahakama kuu katika eneo ambalo limegeuka kuwa makumbusho anasema wademokrats wanatafakari juu ya mipango ya kujaribu kusitisha uteuzi wa rais kwenye baraza la seneti.
Pelosi akifafanua hilo amesema : "Tuna mambo kadha wa kadha tunaweza kufanya. Sitaki kuyazungumzia hapa hivi sasa, lakini ukweli ni kwamba tunachangamoto kubwa katika taifa letu. Huyu rais ametishia hata kutokubali matokeo ya uchaguzi kwa taarifa ambazo yeye na washirika wake wametoa. Kwa hivyo hivi sasa lengo letu kuu na ninadhani Ruth Bader Ginsberg angelipenda tufanya ni kulinda uhakika wa uchaguzi wetu tunapo walinda Wamarekani kutokana na virusi vya corona.
Pelosi na Joe Biden anaegombania kiti cha urais wanafunganisha vita vya mahakama kuu pamoja na jinsi taifa linavyokabiliana na janga la Corona. Na vita vimekuwa vikali kwa sababu mahakama hii ya juu inatarajiwa kuanza kujadili juu ya kuondolewa au la sheria muhmu ya huduma za afya, maarufu Obama Care
"Kwa hivyo Rais anaharakisha mambo ili uamuzi wa aina fulani uchukuliwe, kwa sababu ni novemba 10 ndipo hoja zinaaza kusikilizwa juu ya sheria ya huduma za afya. Hataki kuangamiza virusi anataka kuangamiza huduma za afya," ameongeza kusema Pelosi.
Warepublican wanasema kiti hicho cha mahakama ni muhimu katika kuimarisha uhuru wa kuabudu na masuala mengine muhimu kwa waconservative, kama uhuru wa kumiliki bunduki, uhuru wa kujieleza na kadhalika. Ted Cruz, seneta Mrepuclican kutoka Texas amesema ni muhimu kumteua jaji atakayeheshimu haki za kikatiba.
Cruz anafafanua : "Unaangalia rikodi ya ikiwa huyu mtu ametetea katiba vilivyo, amelinda haki ya kujieleza, amelinda haki ya kuabudu, na kulinda haki ya kumiliki bunduki? Je vyombo vya habari vimemkosoa? Na ameweza kujitetea?
Wademokrats na warepublicans wanakubaliana kwamba huenda kukawa na ugomvi juu ya matokeo ya uchaguzi wa rais na huenda uamuzi ukachukuliwa na mahakama hiyo ya juu ya taifa, kama ilivyotokea 2000. Na ndio maana kuna ugomvi mkubwa sasa kuhusiana na uteuzi huo.
Tunahitaji mahakama kamili siku ya uchaguzi, ukichukulia kwamba kunauwezekano mkubwa wa kuwepo na mashtaka yatakayowasilishwa mahakamani. Tunahitaji mahakama ya juu ambayo itaweza kutoa jibu la uhakika kwa taifa, ameeleza Cruz.
Kilicho wazi hivi sasa kuna tukio jipya katika jukwa la kisiasa lenye utata mkubwa mnamo uchaguzi wa rais ambao pande zote zinakubali lina atahri kubwa kwa nchi nzima.