Trump kusomewa mashitaka yake kwenye mahakama ya Miami Jumanne

Wafuasi wa Trump mjini Doral, Florida Jumatatu.

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump Jumanne anasomiwa rasmi mashitaka kwenye jimbo analoishi la Florida, katika mji wa Miami kutokana na tuhuma za kushikilia hati muhimu za serikali alipoondoka Ikulu ya Marekani mwaka 2021.

Trump anatarajiwa kufika kwenye mahakama ya serikali kuu nyakati za adhuhuri chini ya ulinzi mkali na kusomewa mashtaka yake, na hakimu kutangaza tarehe kesi yake itakapoanza.

Vyombo vya usalama vya serikali vimeimarisha usalama katika mji wa huo vikisema pia kwamba vipo tayari kuzuia ghasia kutoka wa wafuasi wa Trump au makundi mengine yanayopinga wafuasi wake.

Kutakiwa kufika mahakamani kwa Trump kunatokea siku 5 baada ya jopo la mahakama ya Miami kumfungulia mashitaka 37 yakiwemo 31 yanayomtuhumu kushikilia hati muhimu za usalama wa taifa, kinyume cha sheria.

Trump amekuwa rais wa kwanza wa Marekani aliyeondoka madarakani kufunguliwa mashitaka na serikali. Hii ni mara ya pili ndani ya miezi miwili kufunguliwa mashitaka.