Ripoti hiyo ya mwaka 2020 inatoa taswira mbaya ya hali ya mambo duniani, ikieleza kwamba mataifa mengi yamefanya mabadiliko kidogo kabisa au bila ya maendeleo yoyote katika kupambana na janga la rushwa.
Utafiti huo umezingatia zaidi uhusiano kati ya viwango vya rushwa na jinsi mataifa yalivyo kabiliana na janga la virusi vya Corona hapo mwaka 2020. Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Transparency International, Daniel Eriksson anasema wamegundua kwamba rushwa inauwa.
"Mwaka 2020 umeweza kushuhudia uhusiano mkubwa kati ya uwezo wa mifumo ya huduma za afya katika kukabiliana na janga na kiwango cha rushwa katika nchi za dunia. Nchi zilizoko chini kwenye orodha ya CPI zilikuwa na changamoto kubwa kukabiliana na janga hilo kuliko zile zlizoko juu," amesema Eriksson.
Kwa ujumla kati ya nchi 180 zilizofanyiwa uchunguzi, theluthi mbili kati ya hizo hazikupata zaidi ya nukta 50 kwa 100, kwa wastani ilikuwa ni nukta 43.
Kwa wastani nchi za Afrika zilipata pointi 32 ikiwa ni kanda iliyofanya vibaya zaidi chini ya utafiti wa CPI ikionesha kuwepo na maendeleo kidogo sana kulingana na mwaka ulotangulia.
Chini kabisa kwenye orodha hiyo ni Somalia na Sudan Kusini zilizopewa pointi 12 kwa 100, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo ikiwa nafasi ya 11 kutoka chini ilipata pointi 18, wakati Ushelsheli, Botswana na Cape Verde zikiongoza nchi za bara la Afrika.
Tanzania, Senegal, Angola, Ivory Coast na Ethiopia ndizo nchi pekee za Afrika zilizopanda kwa wastani wa nukta 7. Liberia, Msumbiji na Madagascar zimeshuka kwa karibu pointi 7 kwenye orodha hiyo.
Denmark na New Zealand zimechukua nafasi ya kwanza na kuonekana nchi zenye kiwango kidogo kabisa cha rushwa na kupewa pointi 88 kwa 100, zikifuatiwa na Finland, Singapore, Uswisi na Sweden zilizopata nukta 85.