Tetemeko la ardhi limepiga pwani ya kusini mwa Ufilipino

Ramani ya Ufilipino na maeneo jirani na hapo.

Tetemeko hilo lilipiga muda mfupi kabla ya saa kumi na mbili na nusu asubuhi kiasi cha kilomita 20 kutoka kijiji cha Barcelona

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.8 kwa kipimo cha rikta lilipiga pwani ya kusini mwa Ufilipino leo Jumamosi, kituo cha Jiolojia cha Marekani-USGS kilisema, lakini hakuna onyo la tsunami lililotolewa na hakuna ripoti za haraka za uharibifu.

Tetemeko hilo la ardhi lilipiga muda mfupi kabla ya saa kumi na mbili na nusu asubuhi, kiasi cha kilomita 20 kutoka kijiji cha Barcelona mashariki mwa kisiwa cha Mindanao, USGS imesema. Watu wengi walikuwa wamelala wakati walipotikiswa na mitetemeko na kutoka kwenye vitanda vyao.

Shirika linalohusika na matukio ya majanga ya asili kwenye eneo hilo limesema hakuna uharibifu wowote uliotarajiwa kutokana na tetemeko hilo. Katika manispaa ya Lingig, ambako Barcelona iko, afisa anayehusika na majanga, Ian Onsing alisema aliamshwa na tetemeko hilo. “Mtikiso ulikuwa mzito sana. Vitu vilivyokuwepo hapa vilikuwa vinasogea.

Nadhani, tetemeko hilo lilichukua muda wa sekunde 10 hadi15, aliliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu. “Hadi sasa hakuna taarifa za vifo wala uharibifu. Hivi sasa tunafuatilia fukwe kuona kama kuna hali yeyote mbaya.”