Tedros alenga kuongoza WHO kwa muhula mwingine

Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus

Mkuu wa shirika la Afra Duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus Jumanne ameelezea mpango wake wa kukabiliana na janga la corona wakati akishinikiza kuchaguliwa tena kwa muhula wa miaka mitano.

Hayo ameyasema licha ya kupata ukosoaji mkubwa kutoka nchini mwake, Ethiopia kutokana na matamshi yake ya awali kuhusiana na vita vya Tigray. Tedros anayejulikana kwa jina lake la kwanza sawa na wa Ethiopia wengi anawania mhula wa pili kama kiongozi wa WHO bila kupingwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, Tedros ambaye ni kutoka kabila la Tigrinya alikosolewa pakubwa na serikali ya Ethiopia ambayo imekuwa ikikabiliana na vikosi vya Tigray, kutokana na matamshi yake kupitia twitter na kwingineko akishutumu serikali kwa kuzuia upelekaji wa misaada ya kimataifa kwenye eneo hilo.

Tedros alidai kwamba shirika lake lilikuwa limezuiwa kupeleka misaada ya kibinadamu kwenye eneo hilo tangu Julai mwaka jana. Serikali ya Ethiopia kupitia barua ya Januari 14 kwa WHO ililalamikia rasmi matamshi ya Tedros kuhusiana na mzozo kwenye taifa hilo la upembe wa Afrika.