Huku matokeo ya kura ya urais, wabunge na madiwani yakiwa yanaendelea kutolewa kufuatia uchaguzi mkuu wa Tanzania, baadhi ya mawaziri wa serikali wameangushwa na wagombea wa upinzani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Your browser doesn’t support HTML5
Kulingana na matokeo ambayo yamekuwa yakitolewa baadhi ya wabunge wa siku nyingi na machachari wameangushwa katika uchaguzi huu. Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu ambaye alikuwa anawania kuchaguliwa tena kwa tiketi ya chama tawala cha CCM ameshindwa kutetea jimbo hilo dhidi ya mgombea wa chama cha CUF, Abdallah Ali Mtulya na Halima Mdee ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Kawe ameweza kutetea nafasi yake na kurejea tena bungeni kwa kumshinda mgombea wa chama tawala, Kippi Warioba.
John Shibuda mbunge wa muda mrefu ambae amewahi kuhudumu katika nafasi ya ubunge kwa tiketi ya chama tawala, na baadaye alikihamia chama cha upinzani na kuingia tena bungeni kwa tiketi ya Chadema, katika uchaguzi huu alikuwa anatetea kiti chake kwa tiketi ya chama cha upinzania cha TADEA. John Cheyo ambaye aliwahi kugombea urais katika uchaguzi ulopita naye pia ameangushwa.
Kwa upande wa mawaziri na manaibu mawaziri walioshindwa kutetea majimbo yao, ni pamoja na mbunge na waziri wa siku nyingi katika serikali ya Tanzania, Stephen Wassira alikuwa anawania jimbo la Bunda, Christopher Chizza alikuwa anagombea jimbo la Buyungu, Aggrey Mwanry, jimbo la Siha, Anne Kilango Malecela analikuwa anatetea kuwakilisha tena wananchi katika jimbo la Same Mashariki na Godfrey Zambi ameanguka kwa jimbo la Mbozi Mashariki.