Tamasha la filamu la Venice la mwaka huu kufanyika bila nyota wengi kuwepo kutokana na mgomo wa Hollywood

Mcheza filamu wa Marekani Zendaya na mwenzake Timothee Chalamet wakipigwa picha kwenye tamasha la Venice la 2021 .

Tamasha la 80 la filamu la kila mwaka la Venice litafanyika wiki ijayo ingawa mgomo unaoendelea wa Hollywood huenda ukapelekea wacheza filamu wengi kutohudhuria, suala linaloacha macho yakiangazia waelekezi wenye utata kama vile Roman Polanski na Woody Allen.

Tamasha hilo litaanza Jumatano kwenye kisiwa cha Italy cha Venice, na mara nyingi huashiria mwanzo wa kampeni za Oscar pale ambapo nyota wengi hupigwa picha za kupendeza wakati wakiwasili kwa boti maalum za gondola.

Hata hivyo mgomo wa Hollywood ulioitishwa na wacheza filamu pamoja na waandishi ukiwa mkubwa zaidi kwenye tasnia hiyo baada ya zaidi ya miaka 60, una maana kuwa wengi wao wamepigwa marufuku kushiriki kwenye matamsha ya umma.

Miongoni mwa wacheza filamu ambao hawatahudhuria ni pamoja na Emma Stone aliyecheza "Poor Things" na Bradley Cooper aliyeongoza na kucheza filamu ya "Maestro". Licha ya hali iliyopo filamu hizo zingali zinaonyeshwa, wakati waelekezi maarufu wa filamu wakitarajiwa kuhudhuria tamasha la Venice.