Taliban wanaunda mtandao wa kiwango cha juu cha ufuatiliaji wa kamera kwa miji nchini Afghanistan ambao unaweza kuhusisha kurejesha mpango uliobuniwa na Wamarekani kabla ya kuondoka kwao mwaka 2021, msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ameliambia shirika la habari la Reuters wakati mamlaka zikijaribu kuongeza maelfu ya kamera ambazo tayari ziko katika mji mkuu wa Kabul.
Utawala wa Taliban ambao umesema hadharani unalenga kurejesha usalama na kulidhibiti kundi la Islamic State, ambalo limedai kufanya mashambulizi mengi makubwa katika miji nchini Afghanistan, pia limeshauriana na kampuni ya kutengeneza vifaa vya mawasiliano ya China Huawei kuhusu uwezekano wa ushirikiano, msemaji huyo amesema.
Kuzuia mashambulizi ya makundi ya wanamgambo wa kimataifa ikiwa ni pamoja na taasisi maarufu kama vile Islamic State, ni kiini cha muingiliano kati ya Taliban na mataifa mengi ya kigeni, ikiwa ni pamoja na Marekani na China, kulingana na taarifa iliyosomwa kutoka kwenye mkutano.
Lakini baadhi ya wachambuzi wanahoji uwezo wa serikali ya nchi yenye tatizo la fedha kufadhili program hiyo na makundi ya kutetea haki yameelezea wasiwasi wao kwamba rasilimali zozote zitatumika kuwakandamiza waandamanaji.
Maelezo ya jinsi Taliban wanavyokusudia kuongeza na kusimamia ufuatiliaji wa watu wengi, ikiwa ni pamoja na kupata mpango wa Marekani, hayajaripotiwa hapo awali.