Mataifa ya kigeni yalishinikiza Jumatatu kuwahamisha kwa haraka raia wao kutoka Sudan iliyokumbwa na vurugu ambako mapigano makali bado yanaendelea kwa siku ya 10 kati ya vikosi vinavyowatii majenerali wawili waliohasimiana.
Wakati jeshi na vikosi vya kijeshi vikipambana tena mjini Khartoum na kote nchini humo wa-Sudan wenye hofu wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji, chakula, dawa na mafuta pamoja na kukatika kwa umeme na internet, Umoja wa Mataifa (UN) imesema.
Kiasi cha watu 427 wameuawa na Zaidi ya 3,700 wamejeruhiwa kulingana na mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo pia yanaripoti raia wa Sudan wanayakimbia maeneo yalioathiriwa na mapigano wakielekea Chad, Misri, na Sudan Kusini.
Vyumba vya kuhifadhi maiti vimejaa, maiti zimezagaa mitaani, na hospitali ambazo zimezidiwa mara nyingi hulazimika kusitisha shughuli zake kwa sababu za kiusalama alisema Dr. Attiya Abdallah, mkuu wa muungano wa madaktari.