Waziri wa mambo ya nje wa Zambia, Stanley Kakubo amejiuzulu Jumanne, ofisi ya rais ilitangaza saa chache baada ya kukumbwa na kashfa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na shutuma za kufanya biashara na mfanyabiashara mmoja, raia wa China.
Kakubo, ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nje tangu Septemba 2021, alisema katika barua yake kwamba anaacha kazi kwa sababu ya madai mabaya juu ya miamala ya kibiashara. Awali, video ikionyesha watu wawili wakihesabu pesa taslimu zilizokuwa zimetapakaa mezani, zilisambaa haraka kwenye akaunti za mitandao ya kijamii nchini Zambia.
Picha ya ujumbe ulioandikwa kwa mkono wa tarehe 8 Julai 2022, pia iliwekwa mtandaoni. Ujumbe huo uliitaja kampuni ya uchimbaji madini ya China, na kampuni ya uchimbaji madini ya Zambia na kusema kuwa walibadilishana dola 100,000. Ingawa majina ya Kakubo na Zang yalikuwepo kwenye ujumbe huo, haikuwezekana mara moja kuthibitisha maelezo ya kina.
Rais Hakainde Hichilema amekubali kujiuzulu kwa Kakubo, taarifa rasmi imesema. Haikutoa sababu ya kujiuzulu, lakini ikaongeza: “Rais anatambua kazi nzuri na uongozi” wa Kakubo katika serikali.