Serikali ya Tanzania imesema inapitia upya usajili wa meli na kuhakiki taarifa za meli zote zilizosajiliwa nchini humo ili kuondokana na athari za meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania zinazopatikana na makosa katika maeneo mbalimbali duniani...
Makamu wa Rais Samia Suluhuu Hassan amezungumzia hatua ya uhakiki wa meli hizo katika mkutano na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa taarifa kwa wananchi juu ya maazimio yaliyofikiwa katika mkutano ulioshirikisha wataalamu kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano,kushughulikia meli zinazopeperusha Bendera ya Tanzania,kufuatia hivi karibuni kukamatwa kwa meli za Kaluba iliyokamatwa Jamhuri ya watu wa Dominica,ikiwa na takribani tani 1,600 za dawa za kulevya na Andromeda iliyokamatwa Ugiriki ikisafirisha zana zinazotumika kutengeneza silaha kinyume na sheria za kimataifa kwenda Libya.
Serikali ya Tanzania imesema haihusiki na meli hizo zilizokamatwa licha ya kwamba zimesajiliwa nchini kupitia taasisi ya Mamlaka ya usafiri baharini Zanzibar, yenye mamlaka ya kusajili meli za ndani na nje.
Wakati hayo yakiendelea jana wafanyabiashara wawili wakurugenzi wa kampuni tofauti za meli walifikishwa katika mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam wakituhukiwa kupeperusha bendera ya Tanznaia katika meli ya kichina kinyume cha sheria Wafanyabiashara hao ni Issa Haji mkurugenzi wa kampuni ya meli ya Lucky na Abdullah Issa Hanga wa kampuni ya meli ya Saha.