Serikali ya Botswana yakanusha madai ya kuhujumu demokrasia

Rais wa zamani wa Botswana, Ian Khama

Serikali ya Botswana Jumanne imepinga ikisema hayana msingi wowote, madai ya rais wa zamani Ian Khama, kwamba mrithi wake Mokgweetsi Masisi anahujumu demokrasia kwenye taifa hilo ambalo ni dhabiti zaidi kisiasa barani Afrika.

Khama mwenye umri wa miaka 70 ametoa madai hayo kwenye mahojiano ya hivi karibuni na shirika la habari la AFP akisema kwamba Masisi ambaye alimpendekeza yeye mwenyewe amehujumu demokrasia , haki za binadamu pamoja na utawala wa sheria.

Hata hivyo serikali imekanusha madai hayo ikisema kwamba yamechochewa kisiasa kwa nia ya kuharibu jina lake. Khama aliongoza taifa hilo lenye utajiri mkubwa kwa almasi kwa muongo mmoja hadi 2018 kabla ya kuachia Masisi utawala, baada ya kuwa naibu wake kwa muda.

Khama ambaye amekuwa akiishi Afrika Kusini tangu Novemba 2021, amelinganisha Masisi na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, wakati serikali ikisema kwamba inashuku matamshi yake ambayo yametolewa mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika mwaka ujao.

2018, Khama ghafla aliondoka kwenye chama tawala cha Botswana Democratic ambacho baba yake Seretse Khama alikuwa mmoja wa waanzilishi, na kisha akajiunga na upinzani.