Ripoti hiyo ya karibu kurasa 800 imeongeza kusema kwamba takriban nusu yao huenda walikuwa ni watoto. Tume hiyo iliongozwa na mpatanishi mkuu wa Uhispania Angel Gabilondo, ambaye amesema kwamba kanisa hilo limekuwa likikanusha au kuficha ripoti za manyanyaso ya kingono kutoka kwa watu.
Utafiti huo ambao ni wa kwanza rasmi kufanywa na Uhispania dhidi ya makasisi wa Katoliki, pamoja na watu wengine wanaohusishwa na kanisa hilo nchini, umetolewa kufuatia mahojiano 8,000 kwa njia ya simu au mitandao.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, utafiti huo umesema kwamba asilimia 1.13 ya watu wazima waliohojiwa wamesema kwamba walinyanyaswa wakiwa watoto, na makasisi pamoja na watu wengine kama vile walimu wa shule za kidini.
Asilimia 0.6 miongoni mwao walisema kwamba walinyanyaswa moja kwa moja na makasisi. Utafiti huo umefichua kwamba huenda zaidi ya mtu mmoja kwa kila watu 200 nchini Uhispania wamenyanyaswa kingono na makasisi wa kanisa Katoliki.