Rais aliyetolewa mamlakani wa Sudan Omar al-Bashir alifikishwa kortini siku ya Jumanne katika kesi yake iliyoanza kusikilizwa juu ya mapinduzi ya kijeshi ambayo yalipelekea kuchukua madaraka mnamo mwaka 1989.
Akiwa ni rais wa zamani wa jamhuri, Bashir alionekana katika hali nzuri wakati alipotokea akiwa kwenye kizimba cha chuma cha mahakama na amevalia nguo nyeupe za gereza na barakoa aliyoivua ili kujitambulisha.
Baadhi ya washirika wa zamani wa Bashir walionekana pamoja naye kwenye kesi hiyo, ambayo ilikuwa imeahirishwa kwa sababu ya msongamano katika siku ya ufunguzi uliopangwa kufanyika mwezi uliopita.
Maafisa wa jeshi walimwondoa madarakani Bashir Aprili 2019 baada ya maandamano ya miezi kadhaa, na kusababisha makubaliano ya kugawana madaraka kati ya vikosi vya jeshi na raia.
Usikilizaji wa kesi ya Jumanne ilikuja siku moja baada ya uongozi wa mpito wa Sudan kutia saini makubaliano ya amani na baadhi ya vikundi vya waasi ambavyo vilikuwa vikipambana na wanajeshi wa Bashir na wanamgambo washirika huko Darfur.