Raia wa Namibia wazungumzia Rais wao kupelekwa Marekani kwa ajili ya matibabu

Rais wa Namibia Hage Geingob.

Rais wa Namibia amepangiwa kupelekwa Marekani kwa matibabu, baada ya vipimo vya afya kugundua kwamba huenda saratani imerejea tena mwilini, kulingana na taarifa iliyotolewa na ofisi yake Jumatano.

Rais Hage Geingob hapo awali alikuwa amepatikana na celi za saratani ya tezi dume, lakini alitibiwa na kutangazwa kwamba havikuwepo tena mwilini. Hata hivyo baada ya vipimo vya kina vya hivi karibuni mapema mwezi huu, kiongozi huyo aligundulika kuwa na celi za saratani tena.

Mkurugenzi wa shirika la Saratani la Namibia, Rolf Hansen, ameambia VOA kwamba rais amekuwa mwenye uwazi kuhusu matibabu yake saratani ya awali. Amesema kwamba vipimo vya awali vilivyofanywa kwa wakati vilisaidia kwenye matibabu na hatimaye kupona kwa Geingob.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais, kiongozi huyo amekubali mwito kutoka kwa wanasayansi na wataalam wa afya mjini Los Angeles, wa kufanya ukaguzi wa kina wa celi zenye saratani.

Rais huyo amekosolewa pakubwa katika siku za nyuma, kutokana na kutafuta matibabu kwenye mataifa ya kigeni. Hata hivyo madaktari wa Namibia wamekiri kwamba matibabu ya saratani yanahitaji utaalam wa aina yake, na kwamba Namibia haina vifaa wala utaalam wa kukabiliana na ugonjwa huo vilivyo.