Rais wa Malawi asikitishwa na kamati ya Bunge kumkataa mteule wake

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera alipoapishwa kuchukua madaraka mjini Lilongwe, Malawi, June 28, 2020.

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera anasema juhudi za kupambana na ufisadi zitacheleweshwa kwa sababu bunge linakataa kuthibitisha chaguo lake la mkuu wa kuongoza Ofisi ya Kupambana na Rushwa nchini humo.

Akihutubia bunge Jumatano, Rais Chakwera alisema alisikitishwa na kukatishwa tamaa na kamati kukataa jina la mteule wake, Martha Chizuma, siku moja kabla.

Kamati ya Uteuzi wa Umma ya Bunge au PAC ilisema Jumanne Chizuma alikataliwa kwa sababu alishindwa kupata alama zinazohitajika kwa uthibitisho.

Nusu ya wabunge katika kamati hiyo walimpa alama za chini baada ya mahojiano ya tathmini, na matokeo yaliyokusanywa yalionyesha Chizuma akipata alama 15 tu kati ya 25 inayowezekana, chini ya kiwango cha chini cha kufaulu cha 17.

Chakwera aliwataka wabunge, kwa maneno yake, waweke kando maslahi ya kisiasa na ya kibinafsi na wafanye sehemu yao katika kuharakisha mabadiliko ambayo Wamalawi wameyatafuta.

Tangu alipoingia madarakani mwaka mmoja uliopita, Chakwera ameendesha kampeni ya kupambana na ufisadi ambayo imepelekea watu kadhaa muhimu, pamoja na mshauri wa usalama wa Rais wa zamani Peter Mutharika, kukamatwa.

Chakwera anasema anaamini uteuzi wa Chizuma, anayejulikana kama iron lady utasukuma mbele lengo hilo. Chizuma, ambaye kwa sasa ni msimamizi wa masuala ya umma Malawi, aliwaondoa maafisa wakuu watano kwenye nyadhifa zao kwenye kituo cha mdhibiti wa mawasiliano wa Malawi, akisema waliajiriwa kinyume cha sheria wakati wa utawala wa zamani wa Mutharika na chama tawala cha Democratic Progressive Party, au DPP.

Mbunge Ashems Christopher Songwe, ambaye ni wa Chama cha Congress cha Malawi cha Chakwera, alisema Jumatano kwamba kuna madai kwamba wabunge wa upinzani walishawishiwa kupita kiasi kumkataa Chizuma.

Ripoti za vyombo vya habari vya nchi hiyo vilisema moja ya madai moja ni kwamba wabunge wa upinzani walichukua fedha kutoka kwa wafanyabiashara mafisadi ili kupiga kura dhidi yake.

Mchambuzi wa kisiasa Vincent Kondowe anasema kwa kumkataa Chizuma, wabunge hawajafanya makosa yoyote

Wakati huo huo, bunge limepitisha hoja inayoelekeza Kamati ya Uteuzi wa Bunge kuwasilisha ripoti ya kina kwa Bungeni ifikapo Jumanne ijayo juu ya kwanini imemkataa Chizuma.

Wataalam wa sheria wanasema ikiwa uamuzi huo utasimama, rais atawasilisha tena jina la Chizuma au atatangaza mteule mpya.