Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, Ijumaa amewasili kwenye mji mkuu wa jimbo la Sichuan, wa Chengdu, kusini-magharibi mwa China, ili kuhudhuria hafla ya ufunguzi wa michezo ya 31, ya shirikisho la michezo ya vyuo vikuu vya kimataifa, FISU, pamoja na kutembelea China.
Hiyo ni ziara ya kwanza ya Ndayishimiye nchini China baada tangu aliposhika madaraka Juni 2020. Msafara wake unashirikisha waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa maendeleo, waziri wa mazingira, kilimo na mifugo, pamoja na maafisa wengine wa serikali.
Mara kwa mara, rais huyo amekuwa akisema kuwa Burundi inaichukulia China kama rafiki, na mfano mzuri, akielezea kuwa nchi yake ingependa kuendelea kuimarisha urafiki na ushirikiano na taifa hilo, ili kupata maendeleo ya pamoja.