Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, amemfukuza kazi mkuu wa ujasusi aliyehudumu muda mrefu nchini humo, na kumchagua mshirika wa karibu kuchukua nafasi hiyo, shirika la utangazaji la serikali SSBC liliripoti, likinukuu amri ya rais.
Kufukuzwa kwa Akol Koor Kuc ambaye aliongoza kitengo chenye utata cha usalama wa ndani katika idara ya usalama wa taifa (NSS) tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011, imetokea wiki kadhaa baada ya serikali ya mpito kutangaza kucheleweshwa kwa uchaguzi kwa mara nyingine.
Mwezi uliopita ofisi ya Kiir ilitangaza kuongeza muda wa kipindi cha mpito kwa miaka miwili, na kuahirisha uchaguzi kwa mara ya pili kufuatia kucheleweshwa kwa uchaguzi wa mwaka 2022, hatua iliyosababisha ukosoaji kutoka kwa Marekani na wadhamini wengine wa kimataifa, kuhusu mchakato wa amani nchini humo.