Rais wa Marekani Barack Obama amerudia tena nia ya serikali yake kupambana na wanamgambo wa kundi la Islamic State wa nchini Iraq lakini aliwahakikishia wanajeshi Jumatano kwamba hatowapeleka kwenye vita vingine vya nchi kavu huko.
Viongozi wa kijeshi kwenye kituo cha serikali cha jeshi la Marekani huko MacDill Air Force katika jimbo la Florida walimueleza Rais Obama juu ya mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya waasi nchini Iraq. Muda mfupi baadaye alizungumza na wanajeshi na aliwaonya wanamgambo wa Islamic State kuwa Marekani imedhamiria kupambana nao.
“Huu ni wakati wa uongozi wa Marekani. Tutashirikiana na washirika pamoja na marafiki zetu kuwaangamiza magaidi ambao wanatutishia sisi popote wanapojificha kwa sababu katika mtazamo wa haraka wa watu ambao wanajua tu namna ya kuua na kukata viungo na kubomoa, tunaendelea kuongeza na kutoa maendeleo ya hali ya baadaye pamoja na matumaini.”
Jumanne Mwenyekiti wa Wakuu wa Vikosi vya Jeshi, Jenerali Martin Demsey aliliambia jopo maalumu bungeni kwamba kama wanajeshi wa Marekani walihitajika kuwasaidia wanajeshi wa Iraq katika mapambano na waasi ataomba idhini ya Rais Obama.
Lakini Rais alikataa uwezekano huo akiuambia mkusanyiko wa MacDill, “Sitawaweka kwenye vita nyingine ya nchi kavu nchini Iraq”.
Alisema Marekani tayari imefanya zaidi ya mashambulizi ya anga 160 dhidi ya wanamgambo itaendelea kutumia ndege zake za vita kushambulia sehemu za wanamgambo wa Islamic State kama ilivyofanya tena Jumatano. Alisema nchi 40 zinaisaidia Marekani katika operesheni ya kijeshi na kutoa msaada wa kibinadamu kwa wale waliokwama kutokana na visa vya wanamgambo hao.
Wakati huo huo bunge la Marekani linajiandaa kupiga kura juu ya mwito wa bwana Obama wa kutoa silaha na mafunzo kwa makundi ya upinzani yanayopambana na wanamgambo wa Islamic State na kujaribu kumuondoa madarakani Rais wa Syria, Bashar al-Assad. Bwana Obama ameidhinisha mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya maeneo ya kundi la Islamic State nchini Syria lakini Marekani bado haijafanya shambulizi lolote.