Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Rwanda Paul Kagame wamekubaliana juu ya haja ya waasi wa M23 kusitisha mapigano na kujiondoa katika maeneo waliyoteka mashariki mwa Congo, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imesema Ijumaa.
Waasi wa M23 wamefanya mashambulizi kadhaa mashariki mwa Congo mwaka huu, ikiwa ni mara yao ya kwanza kurejea kwa kishindo tangu mwaka 2012, na kusababisha mapigano na jeshi ambayo yamesababisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao tangu mwezi Machi.
Machafuko hayo yalizua mivutano ya kidiplomasia kati ya Congo na nchi jirani ya Rwanda ambapo Congo inaishutumu nchi hiyo kwa kuliunga mkono kundi la M23. Rwanda imekanusha shutuma hizo.
Juhudi za kikanda zinaendelea ili kulegeza uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kumaliza mzozo unaoendelea kwenye mpaka wao.
Kenyatta aliwasili Congo wiki hii kama mpatanishi kwa jopo la wanachama saba wa EAC na mwakilisi wa amani wa Umoja wa Afrika.