Wakati viongozi wa dunia watakapokutana Dubai kuanzia Alhamisi kwa ajili ya COP28, mkutano wa mwaka huu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, wakuu wa mataifa mawili yenye uchumi mkubwa duniani hawatakuwepo.
Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa China Xi Jinping kwa sasa hawana mipango ya kuhudhuria mkutano huo wa wiki mbili ambao unalenga kuziunganisha serikali duniani kuwa nyuma ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) na lengo la makubaliano ya Paris ya mwaka 2015 ya kupunguza hali ya joto duniani hadi nyuzi joto 1.5 juu ya viwango vya kabla ya viwanda.
Nchi zote mbili zitatuma wawakilishi wa ngazi ya juu. Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, mjumbe maalum wa utawala wa Biden kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa atahudhuria. Mjumbe wa masuala ya hali ya hewa wa China, Xie Zhenhua pia anatarajiwa kuwepo.
Miongoni mwa masuala makuu yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni muundo wa mfuko unaoitwa “hasara na uharibifu” unaolenga kuzifidia nchi zenye kipato cha chini ambazo zinakabiliwa na mabadiliko ya hali ya hewa licha ya kuchangia kidogo janga hilo katika vyanzo vyake.