Raila apinga matokeo yanayotangazwa na IEBC

Kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM na mugombea wa urais nchini kenya, Raila Odinga (kulia).

Mgombea urais wa muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, mapema asubuhi ya Jumatano alipinga matokeo ambayo yalikuwa yanaendelea kutangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo, IEBC.

Akihutubia wanahabari mjini Nairobi, Odinga alisema kwamba tume hiyo imekuwa ikitangaza matokeo kwenye tovuti yake bila kufuata utaratibu ufaao.

Matokeo hayo yalianza kutangazwa muda mfupi tu baada ya baadhi ya vituo kufungwa kufuatia kutamatika kwa zoezi la upigaji kura na yalieendelea kumuonyesha rais Uhuru Kenyatta, anayewania awamu ya pili ya urais, akimshinda Odinga.

Kufikia saa moja asubuhi siku ya Jumatano, Uhuru alikuwa anaongoza kwa takriban kura milioni 9.1 huku Odinga akiwa na kura milioni 5.6.

Mwanasiasa huyo wa upinzani mwenye umri wa miaka 72 na ambaye anawania urais kwa mara ya nne, amlisema kwamba matokeo yoyote yanayotangazwa bila kuwepo kwa fomu 34A kutoka vituoni si halali.

Alisema muungano wa NASA hautambui matokeo hayo yaliyokuwa pia yakipeperushwa moja kwa moja na vyombo vya habari.

"Mfumo umeacha kufanya kazi. Sasa ni mitambo inayopiga kura. IEBC wamesema kwamba hakuna chama chochote kilichopinga matokeo. Lakini vyama vitapingaje matokeo bila kujua asili yake? Ni fomu 34A pekee zinazoonesha chanzo cha matokeo," alisema Odinga..

"Kwa hivyo, tunakataa matokeo yote yaliyotangazwa kwa sasa na kuitaka tume ya IEBC itoe fomu 34A za kila kituo kabla ya matokeo zaidi kutangazwa,” aliongeza.

Hata hivyo, tume ya IEBC ilisema hakuna dosari iliyopo na kwamba fomu hizo zitawasilishwa kwa Muungano wa NASA na vyama vingine vya kisiasa, kupitia barua pepe.

Iwapo Odinga atashinda uchaguzi huo, atakuwa rais wa tano wa jamhuri ya Kenya.