Afisa anaeshughulika na safari za anga amesema ndege ya Russia ilioanguka Misri ilipasuka vipande ikiwa hewani siku moja baada ya ndege hiyo ya kampuni ya Metrojet kupoteza mawasiliano ya rada ikiwa kwenye anga ya peninsula ya Sinai ikiwa na abiria 224 ndani yake.
Karibu abiria wote walikuwa ndani ya ndege hiyo ni watalii kutoka Russia waliokuwa wakirejea St. Petersburg wakitoka kwenye mji wa mapumziko wa Sharm el Sheikh.
Raia watatu wa Ukraine ni miongoni mwa waliokufa. Timu za uokozi zimeweza kupata miili 129 pamoja na vifaa vya kurekodia mawasiliano ya ndege maarufu kama Black box.
Kundi la kigaidi linalodai kushirikiana na Islamic State limedai kutungua ndege hiyo lakini wataalam wa safari za ndege pamoja na wale wa kijeshi wanashuku iwapo walikuwa na silaha zenye uwezo wa kuitungua ikiwa umbali wa mita 9,100 angani.
Jumapili rais wa misri Abdel Fattar al-Sisi alisema uchunguzi juu ya ajali hiyo unaweza kuchukua miezo kadhaa.