Polisi nchini Bangladesh walifyatua risasi za mpira na mabomu ya kutoa machozi kuutawanya umati wa watu waliokuwa wakirusha mawe kwenye barabara kuu za mji mkuu Dhaka siku ya Jumamosi katika maandamano ya hivi karibuni ya kumtaka waziri mkuu wan chi hiyo ajiuzulu.
Chama cha upinzani cha Bangladesh Nationalist Party (BNP) na washirika wake wameitisha maandamano kadhaa tangu mwaka jana wakimtaka Sheikha Hasina ajiuzulu na kuruhusu serikali ya mpito kusimamia uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Januari mwaka ujao.
Mapambano yalizuka katika maeneo kadhaa wakati polisi walipoingia kuwatawanya maelfu ya watu waliokusanyika asubuhi na kuzuia usafiri wa magari katika maeneo muhimu ya mji huo. Maafisa kadhaa walijeruhiwa msemaji wa polisi katika mji mkuu wa Dhaka Faruk Hossain ameliambia shirika la habari la AFP.
"Tulifyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira. Takriban maeneo manne ya mji yalishuhudia mapambano kati ya polisi na waandamanaji", Hossain alisema huku maafisa 20 wakijeruhiwa na waandamanaji 90 kukamatwa.