Polisi nchini Nigeria walituma helikopta na boti za kivita wakati upigaji kura ukianza katika majimbo matatu ili kuwachagua magavana huku kukiwa na hofu kuwa ushindani wa kisiasa unaweza kugeuka ghasia.
Uchaguzi wa majimbo una ushindani mkali nchini Nigeria ambapo magavana ni watu wenye nguvu na kwamba suala la mapigano, mauaji na vitisho kwa wapiga kura ni jambo la kawaida. Polisi wameweka vizuizi vya usafiri kwa jimbo la Bayelsa upande wa kusini, Imo huko kusini mashariki na Kogi katikati mwa nchi.
Maafisa wamesema wameimarisha vikosi vya kukabiliana na ghasia za uchaguzi, huku msemaji wa jeshi akisema jeshi linatuma wanajeshi kuimarisha usalama. Haki katika masanduku ya kura inachunguzwa, na pia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilionya kuwa haitahesabu kura kutoka vituo vya kupigia kura ambako mapigano yalizuka.