Papa Francis kuapishwa Jumanne

Baba Mtakatifu mpya Francis akiwa Rome, March 14, 2013.

Baba Mtakatifu mpya Francis anakutana Alhamis na mtangulizi wake kabla ya sala yake ya kwanza kama mkuu mpya wa kanisa katoliki duniani.

Baba Mtakatifu Francis anatarajiwa kumtembelea Baba Mtakatifu wa zamani Benedict ambaye alijiuzulu mwezi uliopita na anakaa kwenye makazi ya viongozi wa kikatoliki nje ya Rome.

Baadaye Alhamis Baba Mtakatifu Francis mwenye umri wa miaka 76 atasalisha ibada kwenye kanisa dogo la Sistine kabla ya makadinali kukutana mjini Rome na baraza linaloshughulika kwa utaratibu wa kumchagua papa.

Jorge Bergoglio ni Mjesuti wa kwanza aliyechaguliwa kwenye wadhifa huo na Baba Mtakatifu wa kwanza kuchukua jina la Francis ataanza kazi rasmi Jumanne.

Wakati huo huo viongozi kutoka duniani kote wanatuma pongezi zao kwa Baba Mtakatifu mpya ambaye pia ni mtu wa kwanza kutoka Latin America kushika wadhifa wa kiongozi mkuu wa kanisa la kikatoliki.

Rais wa Marekani Barack Obama alisifia kuchaguliwa kwa Baba Mtakatifu wa kwanza kutoka bara la Amerika akisema hilo linazungumzia kuelekea nguvu na utendaji wa eneo ambapo alisema inaongeza kujenga dunia yetu. Alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kupeleka salamu za pongezi kwa Baba Mtakatifu mpya ambapo alimuita mpiganiaji wa watu maskini na wasiojiweza.

Makamu Rais Joe Biden ambaye anatoka dhehebu la kikatoliki ataongoza ujumbe wa Marekani kuhudhuria ibada ya kuapishwa kwa Baba Mtakatifu mpya huko Vatican Jumanne ijayo.