Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amekosoa sheria zinazoharamisha mapenzi ya jinsia moja kuwa "zisizo za haki", akisema Mungu anawapenda watoto wake wote kama walivyo na kutoa wito kwa maaskofu wa Kanisa Katoliki wanaounga mkono sheria kuwakaribisha jamii ya LGBTQ kanisani.
"Kuwa mpenzi wa jinsia moja sio uhalifu," Papa Francis alisema wakati wa mahojiano Jumanne na shirika la habari la Associated Press.
Papa Francis alikiri kwamba maaskofu wa Kanisa Katoliki katika baadhi ya maeneo duniani wanaunga mkono sheria zinazoharamisha ushoga au kuibagua jamii ya LGBTQ, na yeye mwenyewe alizungumzia suala hilo katika misingi ya "dhambi." Lakini alielezea mitazamo hiyo kwa asili ya kitamaduni, na amesema maaskofu haswa wanahitaji kupitia mchakato wa mabadiliko ili kutambua heshima ya kila mtu.
"Maaskofu hawa wanapaswa kuwa na mchakato wa uongofu," alisema, akiongeza kuwa wanapaswa kutumia "upole, ukarimu, kama Mungu alivyo kwa kila mmoja wetu."
Baadhi ya nchi 67 au mamlaka duniani kote zinaharamisha vitendo vya ngono ya jinsia moja, 11 kati ya hizo zinaweza au kuweka adhabu ya kifo, kulingana na The Human Dignity Trust, ambayo inafanya kazi ya kukomesha sheria kama hizo. Wataalamu wanasema hata pale ambapo sheria hazitekelezwi, zinachangia unyanyasaji, unyanyapaa na ghasia dhidi ya jamii ya LGBTQ.