Papa Francis anaitembelea DRC siku chache zijazo

Kiongozi wa kanisa Katoliki Duniani Papa Francis

Papa Francis anatarajiwa kuzuru Congo kuanzia Januari 31 hadi Februari 3 ikiwa ni ziara ya kwanza ya Papa tangu mwaka 1985. Maandalizi makubwa yamekuwa yakiendelea katika nchi hiyo kubwa, ambayo ni makaazi ya jamii kubwa sana ya Wakatoliki barani Afrika

Ziara ya Papa Francis nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itaikumbusha dunia kutopuuza mizozo ya miongo kadhaa ambayo imelikumba taifa hilo lenye utajiri wa madini na kuharibu maisha ya mamilioni ya watu, balozi wa Vatican mjini Kinshasa amesema.

Papa Francis anatarajiwa kuzuru Kongo kuanzia Januari 31 hadi Februari 3, ikiwa ni ziara ya kwanza ya Papa tangu mwaka 1985. Maandalizi makubwa yamekuwa yakiendelea katika nchi hiyo kubwa, ambayo ni makaazi ya jamii kubwa sana ya Wakatoliki barani Afrika.

"Congo inayompokea Papa wakati huu si sawa na ile iliyomkaribisha Papa John Paul II miaka 38 iliyopita," Ettore Balestrero, balozi wa Vatican mjini Kinshasa, ameliambia shirika la habari la Reuters.

"Kwa bahati mbaya, kumekuwa na vita na migogoro ambayo inaendelea. Anakuja kuwafariji watu; anakuja kuponya majeraha ambayo bado yanavuja damu."

Alisema taifa hilo la Afrika ya Kati lenye utajiri wa madini lina Wakatoliki milioni 45. Nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama na mizozo tangu miaka ya 1990 ambayo imesababisha vifo vya mamilioni ya watu na kusababisha kuongezeka kwa maelfu ya wanamgambo, ambapo baadhi yao bado wanaendelea na shughuli zao huko.

Papa anatarajiwa kuutembelea mji wa mashariki wa Goma wakati ziara hiyo ilipotangazwa rasmi, lakini mpango wa kufika huko umefutwa kufuatia kuibuka tena kwa mapigano kati ya jeshi na kundi la waasi la M23.

"Congo ni kiini cha kimaadili ambayo hayawezi kupuuzwa," alisema Balestrero.

Papa anatarajiwa kukutana na waathirika kutoka mashariki mwa nchi hiyo hapo Februari 1 pamoja na viongozi wa mashirika ya misaada ya Kikatoliki kulingana na mpango wa ziara yake iliyoelezewa na Vatican.