Wakenya Waangushwa Katika Olimpiki

Mshindi wa marathon Tiki Gelana wa Ethiopia akiwa na Priscah Jeptoo wa kenya aliyeshinda medali ya fedha na Tatyana Petrova Arkhipova wa Russia aliyepata shaba.

Matumaini ya Kenya kujizolea medali katika riadha kwenye mashindano ya Olimpiki yanazidi kudidimia baada ya wanawake na wanaume kushindwa katika mbio ndefu za marathon na mita elfu 10 kwa wanaume

Katika mbio ndefu kwa wanawake Tiki Gelana wa Ethiopia aliibuka mshindi mjini London Jumapili asubuhi baada ya kuwatoka washindani wenzake katika dakika za mwisho huku kukiwa na mvua katika mitaa ya London.

Gelana alishinda mbio hizo na kujipatia medali ya dhahabu katika muda wa saa 2:23:07 ambayo ni rekodi mpya ya Olimpiki. Priscah Jeptoo wa Kenya alipata medali ya fedha baada ya kumaliza sekunde tano tu nyuma ya Gelana. Tatyana Petrova Arkhipova alichukua medali ya shaba baada ya kushika nafasi ya tatu.

Mary Keitany wa Kenya ambaye alikuwa katika kundi linaloongoza kwa muda mrefu alimaliza katika nafasi ya nne katika muda wa 2:23:56, wakati Edna Kiplagat mmoja wa wanariadha aliyetazamiwa kufanya vizuri alimaliza katika nafasi ya 20 katika muda wa 2:27:52.

Kushindwa kwa wakenya katika mbio ndefu kunafuatia matokeo mengine mabaya katika mita 10000 kwa wanawake ambapo Tirunesh Dibaba wa Ethiopia aliwatoka wakenya katika dakika za mwisho na kushinda medali ya dhahabu, Sally Kipyego wa Kenya alichukua medali ya fedha na Vivian Cheruiyot kupata medali ya shaba.

Matokeo yalikuwa mabaya zaidi katika mita 10000 wanaume ambapo wakenya walitoka bila medali baada ya Mo Farah mwingereza mwenye asili ya Somalia kuchukua medali ya dhahabu akifuatiwa na Galen Rupp of Marekani na Bekele Tariku wa Ethiopia. Katika mbio hizo Mkenya Bedan Karoki Muchiri alishika nafasi ya tano na Moses Masai alishika nafasi ya 12. Mganda Moses Kipsiro alishika nafasi ya 10.