Rais Barack Obama amemteua jaji wa mahakama ya rufaa ya serikali kuu Merrick Garland kujaza nafasi ya Mahakama Kuu iliyoachwa wazi baada ya kifo cha Jaji Antonin Scalia mwezi uliopita.
Akitambulika kama mtu mwenye sera za kadiri, Garland, mwenye umri wa miaka 63 kwa sasa ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufaa katika eneo la Washington DC. Maseneta saba Warepublican walioko katika baraza la seneti la sasa ni miongoni mwa wale waliomwidhinisha Garland kushika nafasi aliyo nayo sasa mwaka 1997.
Rais Obama alisema alitafuta jaji ambaye ana misingi mitatu mikuu: "mawazo yaliyo huru, mwenye sifa zisizopingika, na umahiri usiopingwa katika sheria."
Kifo cha ghafla cha Jaji Scalia Februari 13 sio tu kilisababisha upungufu katika mahakama kuu yenye majaji tisa, lakini pia mvutano wa kisiasa baina ya Rais Mdemokrat na Baraza la Seneti linalodhibitiwa na Warepublican.
Saa chache baada ya kufariki kwa Scalia, kiongozi wa Warepublican katika Seneti, Mitch McConnell alisema "nafasi hiyo isijazwe mpaka apatikane rais mpya" na akaahidi kwamba seneti haitaitisha kikao cha kuidhinisha uteuzi wa Obama.
Warepublican wanatumaini kuwa mgombea wao urais atashinda uchaguzi wa Novemba na hivyo kuwa na nafasi ya kufanya uteuzi utakaorejesha mahakama kuu kuwa na wingi wa wakonsevativu.
Obama ambaye atakuwa madarakani mpaka mwishoni mwa Januari 2017, alisema ni wajibu wake wa kisiasa kufanya uteuzi wa mahakama kuu haraka iwezekanavyo.