Niger yasitisha uhusiano na Shirika la Mataifa yanayozungumza kifaransa la OIF

Kundi la mwisho la walinda usalama wa Ufaransa likiondoka Niger. Niamey Desemba 22, 2023.

Maafisa wa kijeshi wa Niger wamesitisha ushurikiano  na Shirika la Kimataifa la mataifa yanayozungumza kifaransa, OIF, wakati likiendelea kuvunja uhusiano wake na Ufaransa, hatua kwa hatua.

Shirika hilo lenye wanachama 88 limekuwa likitumiwa na Ufaransa kama nyenzo ya maslahi yake, amesema msemaji wa utawala wa kijeshi nchini Niger, kupitia televisheni ya taifa Jumapili.

Utawala huo wa kijeshi ulikamata madaraka katika mapinduzi ya mwezi Julai ambayo yalilaaniwa vikali na Ufaransa pamoja na washirika wengine wa Magharibi. Muda mfupi baadaye, utawala wa kijeshi ulivifukuza vikosi vya Ufaransa vilivyokuwa kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi kwa muongo mmoja vikipigana vita dhidi ya uasi wa kiislamu .

Shirika la OIF tayari limesitisha ushirikiano wake na Niger tokana na sababu zinazohusiana na mapinduzi hayo, lakini likasema kwamba lingeendeleza program zinazowanufaisha wananchi moja kwa moja, pamoja na wale wanaochangia kurejeshwa kwa demokrasia nchini humo.