Netanyahu kuwachukulia wahamiaji hatua kali ikiwemo kurejeshwa nyumbani, baada ya maandamano yenye ghasia mwishoni mwa wiki

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa kwenye ofisi yake mjini Jerusalem.Aug. 27, 2023.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kwamba anatafakari kuhusu hatua kali za kuchukua zikiwa ni pamoja na kuwarejesha makwao wahamiaji baada ya maandamano yaliyogeuka ghasia mjini Tel Aviv.

Makundi hasimu ya raia wa Eritrea yalizua ghasia kutokana na misimamo tofauti ya kisiasa ya nyumbani kwao, ambapo baadhi walijeruhiwa pamoja na uharibifu kwa mali. Maandamano yaligeuka ghasia katika mitaa ya Tel Aviv baada ya mamia ya raia wa Eritrea wanaoiunga mkono serikali yao, pamoja na wale wanaoipinga.

Maandamano ya jumamosi yalifanyika wakati wa maadhimisho ya miaka 30 tangu kiongozi wa sasa wa Eritrea kuingia madarakani, wakati wanaoipinga serikali wakiwa wamevaa mashati ya bluu mfano wa bendera ya taifa hilo ya 1952, ikiwa ishara ya kupinga utawala wa kidikteta.

Jumapili waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliitisha kikao cha kamati maalum, ili kujadili suala la waomba hifadhi na wahamiaji nchini humo.