Netanyahu aapa kuendelea na mashambulizi ya Gaza wakati vita hivyo vikifikisha siku 100 tangu kuanza

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Mapigano hayo yalizuka Oktoba 7 kufuatia shambulizi la kigaidi kusini mwa Israel, likiwa baya zaidi kwenye historia ya taifa hilo. Zaidi ya watu 1,200 walikufa ndani ya Israel, wakati takriban wapalestina 24,000 wakiuwawa kwenye Ukanda wa Gaza, kufutia mshambulizi ya Israel.

Wakati Hamas wakiendelea kushikilia zaidi ya mateka 100, hadi watu 120,000 walianza maandamano ya saa 24 mjini Tel Aviv Jumamosi, kuitisha serikali kurejesha mateka wote nyumbani. Zaidi ya mateka 100 waliachiliwa Novemba wakati wa sitisho la muda la mapigano, lakini hakuna wengine walioachiliwa baada ya hapo.

Makampuni mengi pamoja na mashirika ya Israel, Jumapili, ambayo ni siku ya kawaida ya kufanya kazi, yaliadhimisha siku 100 za mapigano hayo kwa kusitisha shughuli kwa dakika 100, kama ishara ya kuunga mkono mateka walioshikiliwa pamoja na familia zao.