Mzozo wa Myanmar unatarajiwa kutawala mazungumzo ya ASEAN

Bendera zinazowakilisha nchi zilizoshiriki mkutano wa ASEAN huko Phnom Penh, Nov. 10, 2022.

Mzozo wa kisiasa wa muda mrefu nchini Myanmar, mivutano katika bahari ya South China na wasiwasi juu ya kuongezeka kwa silaha katika kanda hiyo ni maswali yanayotarajiwa kutawala ajenda wakati wana diplomasia wa juu wa Asia Kusini Mashariki watakapokutana kwa mazungumzo wiki hii nchini Indonesia.

Uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine na ushindani kati ya Marekani na China pia yatajadiliwa ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Qin Gang wanashiriki katika mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, wanaokutana katika mji mkuu wa Indonesia, Jakarta.

Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini, Choe Son Hui hatohudhuria mkutano wa kikanda wa ASEAN, mkutano wa kila mwaka wa usalama, afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Indonesia Sidharto Suryodipuro ameuambia mkutano wa waandishi wa habari Jumatatu, bila kufafanua zaidi.

Pia haijulikani ni nani kati ya watu muhimu katika migogoro ya dunia yenye kuangaziwa zaidi watakutana kando ya mikutano ya mawaziri wa kikundi hicho.