Mwanamuziki wa Ukraine miongoni mwa watu wanaosakwa na Russia

Mwanamuziki Jamala wa Ukaraine anayesakwa na Russia.

Russia imemuorodhesha mwanamuziki wa Ukraine aliyewahi kushinda tuzo za Eurovision 2016 miongoni mwa watu wanaotafutwa, shirika la habari la serikali limesema Jumatatu.

Ripoti zinasema kwamba wizara ya mambo ya ndani ya Russia imemuorodhesha Susana Jamaladinova miongoni mwa watu wanaosakwa kwa kukiuka sheria ya uhalifu.

Mtandao huru wa habari wa Mediazona ambao mara nyingi huangazia taarifa za upinzani pamoja na haki za binadamu umesema kwamba Jamaladinova alishitakiwa chini ya sheria iliyoanza kufanya kazi mwaka jana, ikipiga marufuku kusambaza taarifa za uongo kuhusu jeshi la Russia, pamoja na mapigano ya Ukraine yanayoendelea.

Jamaladinova ambaye jina lake la kisanii ni Jamala ,ni mzaliwa wa kabila la Tatar huko Crimea. Mwaka 2016 alishinda tuzo ya Eurovision kutokana na wimbo wake wa “1994” ukiangazia mwaka ambao Umoja wa Sovieti ulipowafurusha watu wa kabila la Tatar la Crimea.