Mwanaharakati mashuhuri wa LQBTQ nchini Uganda achomwa kisu na watu wasiojulikana

Waandamanaji wapenzi wa jinsia moja wakiwa wamefunika nyuso zao nchini Kenya. Picha ya maktaba.

Mwanaharakati mashuhuri wa haki za wapenzi wa jinsia moja nchini Uganda, ambako kundi hilo limedai kupitia manyanyaso mengi tangu kupitishwa kwa sheria kali dhidi yao mwaka jana, yupo kwenye hali mahututi baada ya kuchomwa kisu mapema Jumatano, shirika lake limesema.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, "Steven Kabuye alichomwa kisu karibu kufa, na watu wasiojulikana, mita chache kutoka nyumba yetu, akielekea kazini asubuhi ya leo,” Shirika lake la Coloured Voices Media Foundation-Truth to LQBTQ limesema kupitia ukurasa wake wa X.

Shirika hilo pia limetoa video ikionyesha Kabuye akiwa kwenye hali ya maumivu mengi, akiwa na jeraha mkononi pamoja na kisu kilichokwama tumboni. Frank Mugisha ambaye pia ni mwanaharakati mashuhuri wa haki za LGBTQ nchini humo amesema kwamba anaamini tukio hilo limechochewa na chuki, kufuatia sheria kali iliyopitishwa, ikiwa moja ya zile kali zaidi ulimwenguni, dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.