Rais Museveni aingia bungeni na kumwapisha spika

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameingia katika historia ya nchi hiyo kwa kuhudhuria uchaguzi wa spika wa bunge na naibu wake na hata kuwaapisha yeye mwenyewe.

Museveni pia amekiri kuwapa wabunge wake shilingi milioni 5 kabla ya uchaguzi wa spika na naibu wake, lakini akasema hatua yake ilikuwa ya uokozi na wala sio ufisadi huku wanasiasa wa upinzani wakiteta kwamba pesa hizo ziliwashawishi wabunge kuwapigia kura spika na naibu wake, kama alivyotaka Museveni.

Mkuu wa sheria na naibu jaji walikwepa kuapishwa kwa viongozi hao wa bunge. Naibu jaji mkuu alitoweka ndani ya bunge baada ya spika Rebbeca Kadaga kuchaguliwa na hivyo Rais Museveni aliingia bungeni na kuchukua kiti cha mbele na kumwapisha spika huyo na hatimaye kuondoa hoja ya wabunge kumzuia Museveni kuingia bungeni.

Wakati wabunge ndani ya bunge hilo walikuwa wakiimba majina ya wagombea nafasi ya naibu spika Jacob Olanya na Nsereko , Nsereko alifukuzwa chama tawala cha NRM , kwa kumpinga rais huyo.

Jacob Olanya alipata ushindi wa naibu spika wa kura 300 dhidi ya 115 za Nsereko wa upande wa upinzani ikionyesha kwamba ameungwa mkono na wabunge wote wa NRM chama tawala na wawakilishi wa jeshi.

Lakini wakati huo huo rais Museveni amesema ni mwenye furaha kwa sababu wabunge wake wamepita mtihani na lililompeleka bungeni ni kuona kwamba iwapo wabunge hao wangepita mtihani huo na kama wangekaidi ushauri wake ingekuwa hujuma kwa chamna chake cha NRM na demokrasia ya Uganda kwa jumla.