Msafara wa wanajeshi wa Eritrea umeonekana ukiondoka katika miji miwili

Mfano wa wanajeshi wa Eritrea katika eneo karibu na Senafe. Februari 17, 2001.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisifu "uondokaji unaoendelea" wa wanajeshi wa Eritrea kama "kiini cha  kupata amani endelevu kaskazini mwa Ethiopia"

Msafara wa wanajeshi wa Eritrea ulionekana ukiondoka katika miji miwili katika mkoa wa Ethiopia uliokumbwa na vita wa Tigray ambako walikuwepo huko kwa takriban miaka miwili iliyopita wakilisaidia jeshi la Ethiopia katika kampeni yake dhidi ya waasi wa Tigray, wenyeji wameliambia shirika la habari la AFP.

Kwa mujibu wa mashahidi wanajeshi wamekuwa wakiondoka Shire na Adwa tangu Ijumaa mchana kwenda mahala kusikojulikana, ingawa baadhi ya wanajeshi walikuwa bado wapo katika miji hiyo miwili siku ya Jumamosi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken siku ya Jumamosi alisifu "uondokaji unaoendelea" wa wanajeshi wa Eritrea kama "kiini cha kupata amani endelevu kaskazini mwa Ethiopia", lakini si mamlaka ya Tigray, wala serikali ya Ethiopia, wala chombo cha kikanda kinachofanya kazi kama mpatanishi, kilichothibitisha kwa shirika la habari la AFP kuhusu kuondoka kwa wanajeshi hao.

"Niliona baadhi ya vikosi vya Eritrea vikiondoka Shire kuelekea kaskazini mashariki. Sijui kama wanaondoka kikamilifu," alisema mkazi mmoja, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Video iliyochukuliwa na mkaazi huyo na kutumwa kwa shirika la habari la AFP ilionyesha malori ya wanajeshi wakitoka nje ya mji huku wakipiga honi za magari na bendera ya Eritrea ikipepea.

Mwananchi mwingine alithibitisha kuona msafara wa malori, mabasi, vifaru na vipande vya silaha vikitoka nje ya mji.