Kikosi cha zima moto nchini Algeria kimekabiliana na moto ambao umewaua watu 34 katika eneo kavu la kaskazini mwa nchi hiyo umeharibu nyumba na maeneo ya pwani pamoja na kugeuza maeneo makubwa ya misitu kuwa maeneo ya taka.
Walioshuhudia tukio hilo walielezea kuta zilizoshika moto haraka ziliusambaza moto huo na picha za televisheni zilionyesha magari ambayo yaliungua, maduka yaliyoteketea kwa moto na mashamba huku maelfu ya wakaazi wakihamishwa.
Moto mkali ulizuka katika misitu ya milima ya mkoa wa Kabylia kwenye pwani ya Mediterania, uliosababishwa na upepo mkali huku kukiwa na joto kali ambalo lilifikia nyuzi joto 48 Celsius siku ya Jumatatu.
Rais Abdelmadjid Tebboune ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu waliofariki, miongoni mwao wanajeshi 10 walionaswa na moto katika eneo la Beni Ksila katika jimbo la Bejaia, kulingana na wizara ya ulinzi ya Algeria.