Mmoja wa wafungwa wa Kipalestina aliyetumikia kifungo kirefu zaidi Israel aachiwa huru

Mfungwa wa Kipalestina wa Israel Maher Younis akikaribishwa kijijini kwake, baada ya kuachiliwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka 40 alhamisi huko Ara, Israel.

Mmoja wa wafungwa wa Kipalestina aliyetumikia kifungo kirefu zaidi nchini Israel Maher Younis, aliachiliwa kutoka jela leo Alhamisi baada ya kukamilisha kifungo cha miaka 40 kwa mauaji ya mwanajeshi wa Israel.

Katika mji wake wa nyumbani, kijiji cha Waarabu wa Israeli cha Ara, Maher Younis alipokelewa kishujaa. Akiwa amevishwa joho la kitamaduni la Kipalestina, alilakiwa na wanafamilia, marafiki na wafuasi kumkaribisha.

Younis na binamu yake Karim Younis walianza kutumikia vifungo vyao mwaka 1983 baada ya wote wawili kukutwa na hatia ya kumuua mwanajeshi wa Israel Avraham Bromberg, ambaye alikuwa akirejea nyumbani kutoka kituo chake.

Wote Maher na Karim wametumikia kifungo kirefu zaidi kwa Mpalestina yeyote katika jela ya Israel, kulingana na Chama cha Wafungwa wa Palestina.

Waarabu huko Israeli ni karibu tano ya idadi ya watu na wengi wao ni wazawa wa palestina ambao walibaki ndani ya nchi mpya ililoanzishwa baada ya vita vyake vya uhuru vya mwaka 1948.