Marekani yaadhimisha miaka 50 ya maandamano ya Washington.

MLK

Wamarekani wanaadhimisha miaka 50 tangu maandamano ya kuelekea Washington na hotuba ya kihistoria “I Have a Dream” iliyotolewa na mchungaji Martin Luther King mbele ya makumbusho ya Rais Lincoln.

Tangu jumamosi maelfu ya Wamarekani wamekuwa wakiwasili katika mji mkuu wa Marekani kuhudhuria sherehe mbali mbali zilizoandaliwa ili kukumbuka siku hii muhimu ya Agosti 28 iliyobadili kabisa ukurasa wa historia na haki za kiraia Marekani.

Siku ya Jumamosi maelfu na maelfu ya wamarekani waliwasili kutoka pembe mbali mbali za nchi hii ili kuiga maandamano yaliyofanyika miaka 50 kumkumbuka kiongozi wa kutetea haki za kiraia aliyeuliwa pamoja na kuwasilisha ujumbe sawa na uliyotolewa wakati ule kuhusiana na maswala mbali mbali ya kijamii.

Watayarishaji na waandamanaji wametoa wito kutaka kutekelezwa maswala mbali mbali, ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, kuanzia haki za wanawake na raia, hadi mageuzi ya uhamiaji, kukomeshwa ghasia za bunduki na kubuniwa nafasi za ajira.

Mbunge kutoka Georgia John Lewis, kiongozi pekee aliyehutubia mkutano huo wa 1963 aliyehai, alizungumzia siku ya jumamosi juu ya maisha magumu aliyokabiliana nayo akiwa Mmarekani mwenye asili ya kiafrika.

"Nilikamatwa mara 40 mnamo miaka ya 60 nilipigwa na kuachwa kwenye damu nikiwa nimezirai. Lakini sijachoka wala siko tayari kukachini na kusema nimeshindwa. Niko tayari kwa vita na vita vitaendelea."

Kwa Marekani wengi wenye asili ya kiafrika ingawa kuna rais mweusi White house wangali wanaamini ndoto haijakamilika. Kijana wake kiongozi aliyeuliwa, Martin Luther King wa Tatu anasema baadhi ya maswala baba yake alipigania yangali ni masuala yenye matatizo makubwa hii leo.

"Hii leo kukiwa na asilimia 12 ya wasiokuwa na kazi miongoni mwa wamarekani wenye asili ya kiafrika na asilimia 38 ya watoto wote wasio wazungu nchini humu wanaishi chini ya kiwango cha umaskini , basi tunajua ndoto iko mbali na kukamilika."

Kutokana na hali hiyo, maandamano yanafanyika kukumbuka malengo yaliyotolewa miaka 50 ilyopita, na kuhamasisha na kuzungumzia changamoto zilizopo.