Mlipuko mkubwa katika kambi ya jeshi nchini Iraq mapema Jumamosi umemuua afisa wa kikosi cha usalama cha Iraq, kinachojumuisha makundi yanayoungwa mkono na Iran.
Kamanda wa kikosi hicho amesema ni shambulizi huku jeshi likisema kuwa linafanya uchunguzi na kulikuwa hakuna ndege za kivita angani wakati wa tukio.
Vyanzo viwili vya usalama vilisema hapo awali kwamba shambulizi la anga lilisababisha mlipuko huo, ambao ulimuua afisa wa kikosi cha uratibu cha PMF na kuwajeruhi wengine wanane huko Kalso, kituo cha kijeshi kilichopo karibu kilomita 50 kusini mwa Baghdad.
Katika taarifa, PMF imesema mkuu wa wafanyakazi Abdul Aziz al-Mohammedawi alitembelea eneo hilo na kukagua maelezo ya kamati za uchunguzi zilizopo mahali ambapo shambulizi limetokea.
Jeshi la Iraq linasema kamati ya kiufundi inafanya uchunguzi wa mlipuko ambao ulitokea saa saba usiku wa kuamkia Jumamosi.