Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema kituo cha matibabu cha Shifa huko Gaza hakifanyi kazi tena kama hospitali na hali katika hospitali hiyo kubwa sana katika Gaza ni mbaya na hatari.
Mkuu huyo wa WHO amesema mashambulizi ya risasi na mabomu kuzunguka hospitali hiyo yamezidisha hali ambayo tayari ni mbaya.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema Jumapili kuwa hakuna sababu ya wagonjwa katika hospitali ya Shifa iliyozingirwa huko Gaza kushindwa kuhamishwa salama, lakini akasisitiza kuwa wanamgambo wa Hamas wanafanya kila wawezalo ili kuwadhuru.
Kiongozi huyo wa Israel amekiambia kituo cha televisheni cha CNN kuwa wagonjwa 100 waliondolewa hospitali na kwamba maelfu ya Wa-palestina wanaoishi katika maeneo ya karibu waliondoka kwa salama katika eneo hilo wakitumia njia salama zinazoelekea kusini mwa Gaza City.