Milipuko yenye nguvu ilitikisa eneo la kuzunguka mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia wa Ukraine Jumamosi jioni pamoja na Jumapili asubuhi, Umoja wa Mataifa umesema, ukimaliza ghafla kipindi cha hali ya utulivu katika kituo hicho.
Timu ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) huko Zaporizhzhia ilisema kuna uharibifu wa baadhi ya majengo, mifumo na vifaa katika kiwanda hicho, lakini hakuna tishio kwa usalama na usalama wa nyuklia. Hakuna ripoti za vifo.
Mkurugenzi mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi alisema katika taarifa jumapili kwamba milipuko hiyo inabainisha haja ya hatua za haraka sana kusaidia kuzuia matukio ya nyuklia huko.
"Habari kutoka kwa timu yetu jana na leo asubuhi zinasumbua sana," alisema Grossi. "Milipuko ilitokea katika eneo la mtambo huu mkubwa wa nyuklia, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo. Yeyote anayehusika na hili, lazima aache mara moja. Kama nilivyosema mara nyingi hapo awali, unacheza na moto!" aliongeza.
Mkurugenzi Mkuu alirudia wito wake wa dharura kwa pande zote mbili katika mzozo huo kukubaliana na kutekeleza eneo la ulinzi na usalama wa nyuklia karibu na ZNPP haraka iwezekanavyo. Katika miezi ya karibuni, ameshiriki katika mashauriano mazito na Ukraine na Russia kuhusu kuanzisha eneo kama hilo, lakini hadi sasa hakuna makubaliano.
Wakati huo huo, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema katika taarifa yake mpya ya kila siku ya ujasusi leo Jumapili kwamba kujiondoa kwa Russia hivi karibuni kutoka Kherson "kulifanywa kwa utaratibu mzuri" na mafanikio yake "huenda ni kwa kiasi kutokana na amri madhubuti ya kiutendaji chini ya Jenerali Sergei Surovikin."