Ofisi ya UN ya kuratibu masuala ya kibinadamu kupitia taarifa imesema kwamba ghasia, na upungufu wa bidhaa, uharibifu, au kukaliwa kimabavu kwa vituo vya afya na mashambulizi kwa wahudumu wa afya vimesababisha athari kubwa kwa maisha ya watu, pamoja na kuzuia uwezo wa kupata huduma za afya.
Shirika la Afya Duniani , WHO limesema kwamba takriban mashambulizi 50 kwenye vituo vya afya yamesababisha vifo 10 na kujeruhi watu 21 tangu mapigano yalipoanza kati ya wanajeshi wa serikali ya Sudan, na vikosi vya Rapid Support Forces, RSF, miezi mitatu iliyopita.
Afisa wa dharura wa WHO kwenye ofisi ya kikanda, Rick Brennan, akizungumza kutoka Cairo, Misri amesema kwamba ghasia hizo zimesababisha ukosefu wa huduma za msingi za afya kama vile kwenye maambukizi ya homa ya mapafu na kuharisha, miongoni mwa mengine.