Meli ya kwanza ya nafaka ikiwa sehemu ya program ya Ukraine ya kupeleka chakula kwa mataifa yanayohitaji, imewasili Jumatatu kwenye bandari ya Djibouti, ili kuanza utekelezaji wa upelekaji chakula kwenye nchi jirani ya Ethiopia ambako ukame mkubwa unaendelea kushuhudiwa.
Ubalozi wa Ukraine nchini Ethiopia umethibitisha kwamba shehena hiyo yenye tani 25,000 za nafaka ni tofauti na program ya shirika la chakula dunia WFP linalofadhili upelekaji wa chakula kutoka Ukraine. Meli ya pili yenye tani 30,000 za ngano kwa ajili ya Ethiopia inatarajiwa kuwasili wiki ijayo huku ya tatu yenye tani 25,000 ikielekea Somalia, kulingana na taarifa kutoka ubalozi huo. Mwezi uliopita rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alitangaza mpango huo, akisema kwamba taifa lake linapanga kupeleka zaidi ya meli 60 kwenye mataifa ya Ethiopia, Sudan, Sudan kusini, Somalia, Congo , Kenya na Yemen miongoni mwa mataifa mengine yanayokabiliwa na ukame.