Mdahalo wa pili wa wagombea urais wa Marekani umefanyika Jumapili katika chuo kikuu cha Washington huko St. Louis huku Mrepublican Donald Trump na Mdemocrat Hillary Clinton wakiingia kwenye ukumbi tayari kupeana changamoto.
Mdahalo wa Jumapili uliongozwa kwa mtindo wa maswali na majibu ambapo wapiga kura ambao hawajafanya maamuzi waliuliza maswali yao moja kwa moja na wengine wakituma kwa njia ya mtandao.
Baadhi ya viongozi wa juu wamemtaka Trump kujiuzulu katika kampeni za kuwania urais baada ya mkanda wa video uliorekodiwa mwaka 2005 kuvuja huku akionekana kutoa maneno ya kuzalilisha kwa mwanamke mmoja aliyetamani kuwa na uhusiano nae kimapenzi.
Clinton aliyeonekana kuwa mtulivu alisema wakati anapinga vikali kuhusu sera za wa republican wengine waliowahi kuwania urais , hii ni mara ya kwanza amewahi kuulizwa kuhusu uwezo wa mgombea kuwa rais.
Licha ya Trump kuomba radhi , Clinton alisema mkanda wa video umeonesha wazi jinsi mpinzani wake alivyo na tabia ya kuwanyanyasa wanawake na kuwadhalilisha .
Maswala mengi yaliulizwa ikiwemo kuhusu wakimbizi wa Syria ambao rais Brack Obama katika utawala wake amependekeza nia ya kuwapokea nchini Marekani.
Trump amelipinga hilo akisema linaweza kusababisha ukosefu wa usalama nchini, lakini Clinton amesema ni vyema kujali wanawake na watoto wanaotaabishwa na vita huku wakishindwa kujitetea na Marekani ni muhimu kuchukua jukumu.
Kuhusu suala la waislamu kupigwa marufuku nchini Marekani kama alivyodai Trump hapo awali, Clinton amesema kama atachaguliwa kuwa rais halitokuwepo, wakati Trump amesema uchunguzi utafanywa kabla ya waislamu wenye msimamo mkali kuruhusiwa kuingia nchini .