Muigizaji amshitaki aliyetengeneza filamu iliyozusha maandamano

Maandamano yalivyokuwa Lebanon

Mchezaji sinema mwanamke aliyetokea katika filamu iliyozusha maandamano ya waislamu sehemu kadha duniani amefungua mashitaka dhidi ya mtengenezaji filamu hiyo kwa udanganyifu.

Katika madai hayo, yaliyofunguliwa mjini Los Angeles, muigizaji Cindy Lee Garcia anadai kuwa mtengenezaji filamu hiyo The Innocence of Muslims, Nakoula Basseley Nakoula, alimhadaa kwa kumwambia kuwa anatokea katika filamu inayoonyesha maisha ya zamani Misri. Lakini maneno waliyotumia wakati wa kupiga filamu hiyo yalibadilishwa na maneno ya kumkashifu Mtume Muhammad.

Garcia anasema amepata vitisho kadha vya kuuawa tangu toleo fupi la filamu hiyo litolewa katika mtandao wa Internet na anashindwa kuonana na familia yake kwa hofu kwamba wanaweza kudhuriwa.

Muigizaji huyo pia anaishitaka YouTube, mtandao unaoonyesha filamu hiyo, na kampuni yake mama Google, kuzitaka ziondoe filamu hiyo katika mtandao, kwa madai kwamba haki yake binafsi imeingiliwa.