Mbunge wa Upinzani wa Zimbabwe atekwa nyara

Wafuasi wa kiongozi wa upinzani wa Chama (CCC) Nelson Chamisa katika mkutano wao wa mwisho wa kampeni Agosti 21, 2023. ZIMBABWE-POLITICS-ELECTION

Mbunge mmoja wa upinzani nchini Zimbabwe ametekwa nyara na watu wasiojulikana mapema Jumatano na kisha kutupwa takriban kilomita 50 kaskazini mwa mji mkuu Harare, wanachama wa chama chake wamesema.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Takudzwa Ngadziore mwenye umri wa miaka 25 na ambaye ndiye mbunge kijana zaidi kutoka chama cha Citizens Coalition for Change, CCC, aliweka video mubashara kwenye Facebook, ikionyesha mwanamme akikimbia kuelekea alipokuwa, akiwa ameshika bunduki aina ya riffle, kabla ya video hiyo kukatizwa ghafla kwa sekunde 7.

Baadaye mjumbe huyo amepatikana karibu na migodi iliyopo kwenye kijiji cha Mazowe akiwa amechapwa vibaya na kuachwa uchi, huku akichomwa kwa sindano ilikuwa na kemikali isiyojulikana, ameongeza kinara wa chama chake bungeni Amos Chibaya. Msemaji wa CCC Promise Mkwananzi amethibitisha tukio hilo, akiongeza kwamba watawasilisha ripoti kwa polisi.