Mbunge wa Italy adai kuna takriban wahamiaji laki saba, Libya, wanaosubiri kwenda Ulaya kupitia bahari ya Mediterranean

Picha ya wahamiaji wakiwa kwenye boti kuelekea Italy kwenye bahari ya Mediterranean

Ripoti za kijasusi zimeonyesha kwamba karibu wahamiaji 700,000 wapo nchini Libya wakisubiri nafasi ya kuingia nchini Italia kupitia kwenye bahari ya Mediterranean.

Ripoti hiyo ni kutoka kwa mbunge kutoka chama cha waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni cha mrengo wa kulia. Hati hivyo idadi hiyo kulingana na afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa, siyo ya kutegemewa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, Tommaso Foti ambaye ni kiranja wa bunge la chini, kutoka chama cha Brothers of Italy, Jumapili ameambia kituo cha televisheni cha Tgcom24, kwamba idara ya kijasusi ya Italia inakadiria kuwa takriban wahamiaji 685,000 waliopo Libya, wengi wao wakiwa wamezuiliwa kweye makambi, wanasubiri kwa hamu kuingia ulaya wakitumia boti, zinazobeba wahamiaji haramu, kupitia bahari ya Mediterranean.

Waziri mkuu wa Italy anatarajia kwamba mkutano wa Umoja wa Ulaya baadaye mwezi huu utashugulikia tatizo la idadi kubwa ya wahamiaji na waomba hifadhi wanaoingia kwenye mataifa kama vile Ugiriki, Cyprus, Malta, Spain na Italy kupitia kwenye bahari ya Meditarranean. Kwenye ripoti nyingine, wahamiaji 30 wanaendelea kusakwa huku wengine 17 wakiokolewa takriban kilomita 180 kutoka ufukwe wa Libya, baada ya boti yao kuzama walipokuwa wakijaribu kuokolewa na meli kubwa, walinzi wa bahari wa Italia wamesema Jumapili usiku.

Wamesema kwamba kutokana na kuwa boti hiyo ilizama karibu na Italia, meli nyingine kadhaa za uokozi za taifa hilo zinasaidia kwenye shuguli za uokozi. Boti ya uokozi iliyobeba manusura 17 waliookolewa iliwapeleka Italia ingawa ingesimama Malta kwanza ili kushusha wawili waliokuwa wanahitaji huduma za dharura za afya.